Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Wizara ya Ulinzi ya Israel imesaini mkataba wa thamani ya mabilioni kadhaa ya dola na kampuni ya ndani ya Rafael kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mfumo wa ulinzi wa anga wa Gombo la Chuma (Iron Dome).
Wizara hiyo imesema katika taarifa kuwa Meja Jenerali (mstaafu) Amir Baram, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Israel, ametia saini mkataba mpya wa ununuzi ambao utaongeza uzalishaji wa mfumo huu wa ulinzi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa mujibu wa mkataba huu, kampuni ya Rafael itawasilisha idadi kubwa ya makombora ya kukinga ya Iron Dome kwa Shirika la Ulinzi wa Makombora la Israel na kwa Jeshi la Israel.
Wizara ya Ulinzi ya Israel imekumbusha pia kuwa kifurushi cha misaada ya Marekani chenye thamani ya dola bilioni 8.7, ambacho Bunge la Marekani lilipitisha mwezi Aprili 2024, kinajumuisha dola bilioni 5.2 kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel. Mifumo hiyo inajumuisha Iron Dome, Davids Sling (Falaqhun Dawud), na mfumo wa ulinzi wa anga wa miale ya leza wenye nguvu kubwa ambao uko katika hatua ya mwisho ya maendeleo.
Taarifa hiyo haikubainisha kiasi mahsusi cha Iron Dome ndani ya fedha hizo, lakini imesisitiza kuwa mkataba uliosainiwa una thamani ya mabilioni ya dola.
Yoav Gallant, Waziri wa Ulinzi wa Israel, amesema katika taarifa hiyo:
“Mkataba huu utakuwa hatua ya kimkakati itakayoongeza uwezo wetu wa kujilinda angani dhidi ya maadui, na pia ni uthibitisho wa kina wa uimara wa ushirikiano wetu na Marekani, pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizi mbili.”
Israel ina mifumo kadhaa ya ulinzi wa makombora, ikiwemo Iron Dome kwa ajili ya makombora ya masafa mafupi na ya kati, Davids Sling, na Arrow System kwa makombora ya masafa marefu.
Katika kipindi cha miaka miwili ya vita dhidi ya Gaza, Israel ilitumia kwa kiwango kikubwa mifumo yake ya ulinzi wa makombora, ikiwemo Iron Dome, kukabiliana na makombora yaliyokuwa yakirushwa kutoka Gaza, Lebanon, Yemen na Iran. Hata hivyo, ripoti zinaonyesha kuwa mifumo hii ilishindwa mara kadhaa.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa tarehe 10 Oktoba yalihitimisha miaka miwili ya mashambulizi ya Israel ambayo yalianza tarehe 8 Oktoba 2023 kwa msaada wa Marekani, na kusababisha kuuawa zaidi ya Wapalestina 69,000, kujeruhiwa zaidi ya 170,000, na kuharibu asilimia 90 ya miundombinu ya kiraia ya Gaza.
Kwa miaka mingi Israel imekuwa ikikitangaza Iron Dome — mradi wa pamoja na Marekani — kama mfumo uliofanikiwa katika kukabiliana na makombora ya masafa mafupi na ya kati. Hata hivyo, mfumo huo umeshindwa mara kadhaa, ikiwemo katika vita na Iran mwezi Juni uliopita, na kushindwa kulinda anga ya Israel.
Aidha, Februari iliyopita, uchunguzi wa ndani wa jeshi la Israel ulionyesha kuwa mfumo wa ulinzi wa makombora ulianguka kabisa katika saa za mwanzo za shambulio la tarehe 7 Oktoba 2023. Katika siku hiyo, makundi ya Kipalestina — hasa Hamas — yalifanya shambulio la kushtukiza dhidi ya vitongoji na kambi za kijeshi za Israel, na kusababisha kuuawa na kutekwa kwa idadi ya wanajeshi na walowezi wa Israel, ambao baadaye walipelekwa Gaza; shambulio ambalo lilikuwa jibu kwa uvamizi endelevu wa Israel dhidi ya Wapalestina na Msikiti wa Al-Aqsa.
Your Comment